Jumanne 30 Septemba 2025 - 14:52
Kwa Amali hii mshindeni shetani

Hawza/ Qur’ani Tukufu kwa kusisitiza juu ya maneno mazuri, inatufundisha kwamba kauli nzuri si tu kwamba inapanda mbegu za mapenzi katika nyoyo, bali pia inazuia unafiki na uadui, kinyume chake kauli mbaya ni silaha mikononi mwa shetani inayoharibu mahusiano.

Shirika la Habari la Hawza - Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Qur’ani Tukufu:

(وَقُولُوا لِلنَّاسِ حُسْنًا)

“Na semeni na watu kwa wema.” 1

Sherehe:
Qur’ani Tukufu na Ahlul-Bayt wametoa umuhimu maalumu kwa mahusiano na mapenzi baina ya watu, na kwa sababu hiyo wakamuusia mwanadamu ashike kila jambo linaloimarisha mahusiano na mapenzi hayo, moja ya mambo hayo ni kutumia maneno mazuri.

Maneno mazuri yanaweza kupanda mbegu za mapenzi ndani ya nyoyo za watu na kuimarisha uhusiano wao.

Lakini kinyume chake, maneno mabaya na yasiyopendeza yanaweza kuwa chombo mikononi mwa shetani ili kupanda mbegu za chuki na unafiki katika nyoyo na kugeuza ahadi za urafiki na mapenzi kuwa uadui.

Kama ambavyo Qur’ani katika aya nyingine inasema:

(وَقُلْ لِعِبادِی یَقُولُوا الَّتِی هِی أَحْسَنُ إِنَّ الشَّیْطانَ یَنْزَغُ بَیْنَهُمْ إِنَّ الشَّیْطانَ کانَ لِلْاءِنسانِ عَدُوّا مُبِینا)

“Waambie waja wangu waseme maneno mazuri, maana Shet'ani huchochea ugomvi baina yao. Hakika Shet'ani ni adui aliye dhaahiri kwa mwanaadamu..” 2

Amirul-Mu’minin (a.s) naye amesema kuhusu jambo hili:

(سُوءُ اَلْمَنْطِقِ یُزْرِی بِالْقَدَرِ وَ یُفْسِدُ اَلْأُخُوَّةَ)

“Maneno mabaya huchafua heshima na huharibu undugu.” 3 

Kwa hivyo, iwapo mtu hatailazimisha nafsi yake kusikiliza maneno ya Mwenyezi Mungu, yaani akapuuza usia wa Mungu kuhusu hulka njema, shetani hutumia fursa hiyo na si tu humfanya mtu mwenye maneno mabaya kuwa hana heshima na hadhi, bali pia huvunja ahadi za mapenzi baina yake na waliomzunguka.

Hii ndiyo sababu kwamba chochote kinachoweza kuwa chombo mikononi mwa shetani na wafuasi wake kinapaswa kuepukwa.

Hoja ya kiakili juu ya maneno mazuri na kujiepusha na maneno mabaya

Ikiwa mtu atatuuliza: “Wakati wa kukutana na wengine, je, mnapenda mhutubie kwa maneno mazuri, au kwa maneno machafu na yasiyopendeza?” Jibu letu litakuwa lipi?

Hakika hakuna mtu yeyote anayependa wala kuridhia ahutubie kwa ukorofi na maneno ya dharau. Hivyo basi, ikiwa tunatarajia kwenye nafsi zetu mahusiano ya namna hii, kwa nini tusitende vivyo hivyo tunapokutana na wengine?

Imam al-Baqir (a.s) pia ametufundisha jambo hili kwa kusema:

(قُولُوا لِلنَّاسِ أَحْسَنَ مَا تُحِبُّونَ أَنْ یُقَالَ فِیکُمْ)

“Semeni kuwaelezea watu maneno bora kabisa ambayo mnapenda yasemwe juu yenu.” 4

Rejea:
1. Surat al-Baqara, aya ya 83.
2. Surat al-Isra, aya ya 53.
3. Ghurar al-Hikam, j. 1, uk. 402.
4. Tafsiri Nur al-Thaqalayn, j. 1, uk. 94.

Imeandaliwa na kitengo cha Elimu Utamaduni cha Shirika la Habari la Hawza.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha